Header Ads

SAA NANE KABLA YA STARS KUIKABILI CHAD,MKWASA ANENA HAYA

IMG_7330

ND’JAMENA,CHAD


TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, leo inashuka Uwanja wa Ommisports Idriss Mahamat Ouya jijini ND’jamena kuwavaa wenyeji Chad katika mchezo wa kuwania fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Kikosi cha Stars kikiongozwa na Kocha Mkuu Charles Mkwasa kiliwasili nchini humo kwa ajili ya mchezo huo muhimu kuhakikisha wanapata ushindi wa ugenini kabla ya kurudiana Machi 28, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

IMG_7443

Taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto ilimkariri Mkwasa akisema wamejipanga vizuri na wanatarajia kung’ara leo.

“Tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo huu wa ugenini ili tutakaporudi nyumbani tutumie pia vyema uwanja wetu, ” alisema Mkwasa.

Licha ya kukabiliwa na mchezo huo muhimu, kikosi cha Taifa Stars kiliwasili kwa mafungu kutokana na wachezaji wengi kukabiliwa na majukumu katika timu zao, ambapo zilikuwa kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho mwishoni mwa wiki.

Kwa mujibu wa Kizuguto, kikosi cha Taifa Stars kimekamilika baada ya kuwasili kwa nahodha wa timu hiyo anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta na mshambuliaji Thomas Ulimwengu anayecheza TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taifa Stars inakutana na Chad ambayo si miongoni mwa nchi zinazojulikana katika soka, ikiwa inashika nafasi ya 127 katika ubora wa viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), huku Tanzania ikiwa ni ya 125.

Hadi sasa Taifa Stars inashika nafasi ya tatu katika kundi hilo la G ikiwa imecheza mechi mbili ikiwa na pointi moja, ambapo ya kwanza ilifungwa mabao 3-0 na Misri mjini Cairo, kisha ikatoka 0-0 na Nigeria Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Misri inaongoza Kundi G ikiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi zote mbili ikiifunga Taifa Stars na Chad, wakati Nigeria inashika nafasi ya pili baada ya kuifunga Chad na kutoka sare na Taifa Stars, huku Chad yenyewe ikiburuza mkia baada ya kupoteza mechi zote mbili ilizocheza.

Kwa mazingira hayo ni wazi Taifa Stars ina kila sababu ya kushinda leo na kujiweka katika nafasi nzuri katika michezo ya marudiano kwa kundi hilo.



No comments

YoungGskillz.com . Powered by Blogger.